Ilikua ni ndoto ya Baba yangu, siku moja akistaafu angenunua nyumba nzuri ya kuishi, wazo hili lilitupatia tabasamu katika nyakati zake za mwisho kazini. Alifundisha shule ya Msingi kwa Miaka zaidi ya 20, macho yake yalichoka kwa vumbi la Chaki. Alizeeka haraka kuliko ilivyokadiriwa, alibahatika kuowa Mke mzuri mwenye kuipenda familia.
Baraka nyingine ilikua ni kunizaa Mimi, walinipa jina la Celin, lilikua ni jina la marehemu Bibi yangu. Japo mwanzo Mama alikua hataki majina ya kurithi lakini Baba alisistiza hadi jina likakubalika, Mimi ndiye Celin.
Mara zote Baba yangu hujivunia Mimi, nimerithi akili za Baba yangu. Njia yangu ilionekana mapema sana nikiwa na Miaka saba, Baba alipambana kunisomesha kwa Mshahara wake mdogo hadi nikafika chuo Kikuu. Nilisafiri kwa ajili ya Masomo ya Chuo Kikuu maarufu Nchini. Nikiwa nakaribia Likizo yangu, siku moja Baba alinipigia simu.
Ilikua majira ya Usiku, nilikua nimejilaza kitandani nikiutafuta Usingizi, niliposikia simu yangu ilikua ikiita. Mara moja niliipokea nikiwa mwenye furaha kubwa sana
“Celin” Baba aliniita kwa sauti ya furaha, nilihisi ana jambo fulani la kuniambia. Nilitabasamu huku nikimtaka Baba aliseme jambo hilo haraka sana.
“Mwanangu, Pesa za mafao yangu zimeingizwa jioni ya leo. Nilisubiria muda ambao ungekua umemaliza pirika zako ili nikueleze” Baba alisema kwa sauti ya Ubaba ambayo ilinifanya nijione Mimi ni Mtu muhimu sana kwake.
“Enhee‼”
“Mimi na Mama yako tumekaa tumefikiria sana, tumeona ni bora tuwe karibu na wewe. Si unaikumbuka ndoto yangu?” Baba aliniuliza, nisingeliweza kuisahau ndoto yake ya kununua nyumba lakini nilijiuliza wanahitaji kuwa karibu na Mimi kivipi.
“Siwezi kusahau Baba, lakini mnataka kuwa karibu nami kivipi?”
“Tunahamia Mjini, Mjomba wako Mgina ametuambia kuwa atatusaidia kupata nyumba huko. Hatutaki tena kuishi Kijijini” Nilichokisikia kiliamsha furaha yangu kwa kiasi kikubwa sana, sikuamini. Nilipiga kelele kwa furaha sana
“Baba unajua siamini kabisa Kama itatimia hivi karibuni”milisema kwa shahuku kubwa sana.
“Amini Binti yangu, tayari nyumba imepatikana. Mjomba wako atakupigia simu kesho ukaiangalie, kama ni nzuri utatuambia ili tufanye malipo, Mimi na Mama yako tuje mara moja Mjini” Kiukweli siwezi kuficha, mazungumzo haya yalikua ndio mazungumzo ya furaha zaidi kuwahi kunisisimua kiasi cha kupagawa.
Kwa kipindi cha Mwaka Mmoja na miezi kadhaa nilitengeneza marafiki ambao walikua wakiishi Mjini, ilinipa uhakika wa kuendelea nao endapo tutapata nyumba ya Kuishi. Siku yangu iliisha ikiwa imeniacha na furaha sana.
Mwanzo wa kila kitu.
Siku iliyofuata niliamka mapema sana, nilijiandaa huku nikiweka simu yangu kando yangu kila dakika nikiichungulia kama Mjomba Mgina alikua akipiga. Majira ya saa tatu asubuhi alinipigia, niliipokea kwa shahuku kubwa sana, nilisimama kando ya dirisha huku nikiangalia mandhari ya nje iliyojaa Miti mirefu na Bustani kadhaa.
“Celin, uko tayari?” aliniuliza baada ya salamu, jibu langu lilikua ndiyo.
“Nakutumia Namba ya Dalali, bahati mbaya siwezi kufika. Japo nilipendelea niwepo lakini naamini unaweza ukafanikisha ndoto ya Baba yako” alisema.
“Hakuna shida Mjomba, Tayari mimi ni mwenyeji hapa Mjini. Nina uhakika na hilo, ondoa shaka” nilimjibu kwa sauti yangu laini iliyojaa adabu niliyofundishwa na wazazi wangu. Baada ya simu kukatika, mara moja namba ya Dalali iliingia kwenye simu yangu, ilikua ni hatua moja mbele kuelekea kutimiza ndoto ya Muda mrefu ya Baba yangu.
Nilipozungumza na Dalali, alinielekeza ni wapi tutakutana. Alipendelea tukutane njia panda ya kuelekea Benki ya Taifa. Nilichukua Taxi kuelekea huko huku nikiwa na shahuku kubwa sana, kichwani mwangu nilijenga taswira ya aina ya nyumba ambayo nitaoneshwa.
Tabasamu halikukauka usoni pangu hadi tunafika Njia panda. Nilimlipa dereva pesa yake kisha niliteremka na kuangaza huku na kule kabla ya kumpigia, alinipungia mkono akiwa kando ya barabara. Nilisogea hapo kisha tulitumia Pikipiki moja, haikua ajabu sababu ni usafiri wa kawaida sana.
Alinipeleka mtaa mmoja uliotulia sana, mandhari tu ya mtaa yalinivutia sana. Palikua kimya bila kelele za aina yoyote ile, kisha tulitembea kidogo baada ya kushuka kwenye Pikipiki. Dakika tano baadaye tulisimama nje ya nyumba moja ya ghorofa moja.
Haikua nyumba niliyoitegemea, japo ilikua nzuri sana kwa nje. Ilikua na Bustani nzuri na hali ya hewa ya kuvutia macho na Masikio. Nilisisimka kidogo kisha nikaomba nipelekwe ndani ya nyumba hiyo iliyojengwa kwa Mtindo wa ajabu kidogo, ilionekana ni nyumba ambayo yenye mtindo wa nyumba za Ughaibuni. Ilikua na asili ya Uingereza hivi,ilikua rahisi kwangu kugundua hilo sababu nilikua nasomea masomo ya Mazingira na usanifu wa Majengo.
“Hii nyumbaa‼” nilitamani kumuuliza dalali, jambo lililonijia kichwani ni asili ya hiyo nyumba. Aliniwahi kama vile alikua kichwani kwangu, alinijibu haraka tena kwa ucheshi wa Kibiashara kama ilivyo kawaida yao.
“Iko tofauti sana na nyumba za Mtaa huu, ni hii pekee imejengwa kizungu zaidi. Usijali, hii nyumba ilijengwa Muda mrefu kidogo lakini bado inavutia sana, ina uimara pia mazingira yake ni kama unavyoyaona” alikua akiongea huku akiitupa mikono yake kunionesha huku na kule, aliyazungusha macho yake kama Pia hivi, hata hivyo nilitabasamu kisha akaendelea kunizungusha.
Baada ya kuzunguka maeneo ya nje nilianza kubadilisha mtazamo wangu juu ya nyumba hii, nilianza kuipenda, tukaingia ndani. Tulizunguka kila mahali, nilikubaliana na dalali kua ilikua ni nyumba nzuri sana ambayo hata Baba yangu angeipenda. Pale pale nilimpigia simu Baba na kumweleza kua ni nyumba nzuri ya ghorofa moja. Baba aliniuliza mara mbili mbili kama kweli nilikuwa nimeipenda
“Baba ni nzuri sana, ina hewa. Mazingira yake yametulia sana kuliko nilivyofikiria mwanzo” nilisema huku nikiwa nimesimama kando ya Dirisha kubwa la juu.
“Kama wewe Celin umeipenda basi nitazungumza na Mjomba wako, kila kitu kitaenda sawa. Hesabia kua hiyo ni nyumba yetu mpya” alisema Baba.
“Unanisisimua Baba, ngoja niangalie zaidi Basi” Nilimuaga Baba, Nikiwa na tabasamu tele machoni pangu nilianza kuhisi hali fulani ya ajabu. Nilihisi kama nyuma yangu palikua na Mtu mkubwa anayekuja taratibu, kivuli chake kilikua kinanisogelea na kwa hakika nilikiona kwa macho yangu kupitia jicho la wizi.
Nilijawa na hofu sana, niliamua ni bora nigeuke nione ni Nani aliyekua nyuma yangu. Niligeuka haraka kwa hofu sana, hapakua na yeyote yule isipokua nilisikia sauti ya Dalali akiniuliza kama nilikua tayari nimemaliza kuongea na simu.
Nilishusha pumzi zangu, kichwani mwangu na moyoni mwangu nilijiambia ilikua ni hisia mbaya ya ghafla. Mara aliingia Dalali, nilijitahidi kujiweka sawa nisimuoneshe wasiwasi wowote ule. Hata hivyo sikua na uhakika na hisia zangu, nilichowaza kilipotelea mawazoni, sikutaka kukipa kipaumbele, niliachia tabasamu
“Nimemaliza” nilimjibu, alikua tayari amenisogelea
“Anasemaje?” aliniuliza
“Atawasiliana na Mjomba Mgina, halafu watarudi kwako kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mauzo. Samahani, hii inagharimu pesa ngapi?” nilimuuliza, muda wote tulikua tunazunguka bila hata Mimi kujua nyumba ilikua inauzwa shilingi ngapi
“Mwenye Nyumba anataka Milioni 84 tu, ameishusha bei ili aiuze. Kama mtachelewa kidogo basi inaweza kuuzwa maana ipo sokoni sana” alisema Dalali, nilizungusha macho yangu kuitathmini upya. Namna ilivyo na kiasi kilichotajwa vilikua mbingu na ardhi. Nyumba nzuri kiasi kile, tena ya ghorofa halafu ipo Mjini iuzwe kwa bei rahisi kiasi kile?
“Vipi mbona kama unatafakari jambo?” aliniuliza, aligundua tafakari yangu. Sikutaka kufanya mambo yawe magumu, nilimwambia
“Hakuna kitu, hakika ni nyumba nzuri sana. Baba atainunua haraka siyo jambo la kujali, pesa ipo mfuko wa shati” yule Dalali alitabasamu kisha akaniambia
“Hamtojutia kuinunua, nawahakikishia” alisema kisha tulishuka chini, kisha tulitoka ndani ya nyumba. Tulianza safari ya kutoka kabisa nje ya uzio. Tulipofika nje kabisa niliangaza huku na kule, nyumba ya Jirani nilimwona Mzee Mmoja aliyevalia Baraghashia, alikua akisoma gazeti.
Alivalia singlendi nyeupe, chini alikua amevalia msuli, nilipomtazama kwa makini niligundua alikua akitutazama kwa macho ya wizi. Nilitamani kujua kwanini alikua akitutazama vile, alikua ameketi kwenye kiti cha kukunja.
Macho ya yule Dalali yalikua kwangu kisha kwa yule Mzee, alionekana ana wasiwasi fulani alioamua kuuficha kwa makusudi, sikujua alikua akificha nini kupitia macho yake. Mara moja yule Mzee alinyanyuka na kuingia ndani, niliporudisha macho yangu kwa dalali alianza kuniambia
“Mazingira ni mazuri sana, mwenye umeona hakuna kelele. Jitahidi sana muichukue”
“Usijali, kwanini yule Mzee alikua akitutazama kwa jicho lile?” sikutaka kuliacha jambo lile hivi hivi, Dalali akaniangalia kama Mtu aliyekua akitafuta cha kuongea kisha akaniambia
“Penye kheri hapakosi husda, naye ni Dalali pia. Hawezi kufurahia pesa ya Udalali ikiingia kwa mwingine, anaihangaikia sana nyumba hii kuiuza” alinipa jibu ambalo lilinifungua kidogo na kunipa mwanga kiasi fulani nikatoka gizani, niliondoa wasiwasi wangu. Basi,tuliachana hapo nikachukua Bajaji kurudi Chuoni nikiwa tayari nina uhakika kua kila kitu kipo sawa.
Kila kitu kilienda sawa, Baba aliinunua ile nyumba kwa bei rahisi sana, alipofika Mjini alishangaa sana kukutana na nyumba nzuri ya ghorofa moja tena iko Mjini. Tulihamia ndani ya Nyumba yetu mpya, Maisha mapya yalianza.
Maisha mapya Mjini yalianza kwa furaha sana, kuwaona Wazazi wangu wakiwa kando yangu ilinipa faraja na nguvu ya kuzidi kusoma kwa Bidii. Baba yangu aliishi kama Mstaafu aliyetimiza malengo yake, aliandaa tafrija fupi kusherehekea Miaka yake ya kazi. Tuliwaalika ndugu jamaa na marafiki walioko Mjini, tuliandaa chakula, nyama choma na vinywaji vya kutosha.
Marafiki zangu Ziada na Caren walifika nyumbani kwetu, waliisifia sana nyumba yetu. Tulifurahi kwa pamoja eneo la Bustani mahali ambapo Tafrija hiyo ilikua ikifanyika. Tafrija ilifanyika Usiku kama saa mbili hivi, ilimlazimu Baba kupanga muda huu ili kutupatia fursa sisi Wanafunzi tuwepo baada ya muda wa chuo kwisha.
Vinywaji vilikua vya kutosha, anayejisikia kunywa soda aligida, anayejisikia kunywa maji kama Mimi naye aligida, wanaopenda bia waligida pia. Muziki wa taratibu ulikua ukituburudisha huku stori za hapa na pale zilikua zikiendelea.
Nikiwa nazungumza na marafiki zangu nilimwona tena yule Mzee wa nyumba jirani, alikua amevalia shati lenye vyumba vidogo vidogo vya rangi nyeusi na nyekundu, alivalia mawani ya macho, alikua amesimama getini. Sikumbuki kama nilimwalika hapo, istoshe hakuna aliyekua amemzoea. Nilishtuka kidogo, nikawatazama Ziada na Caren kisha nikawaambia
“Samahani, nakuja” nilisema huku nikiweka mezani glasi yangu ya soda, lakini ziada akanishika mkono, alikua ametumia kilevi kidogo
“Celin, nahitaji kutumia choo” aliniambia, nilipeleka macho kwa yule Mzee kuona kama alikua pale pale getini, ndiyo‼ alikua amesimama bado akiniangalia bila kutingisha shingo yake, nikayarudisha macho kwa Ziada.
“Pandisha juu, mkono wa Kulia” nilisema, nilimtaka aende mwenyewe ili Mimi nikazungumze na yule Mzee.
“Twende nitamsindikiza, usijali Celin” alisema Caren, niliachia tabasamu la kukubali waende ili nikaongee na yule Mzee, hisia yangu ya ndani ya moyo wangu iliniambia jambo moja kuhusu yule Mzee.
“Kuna jambo huyu Mzee analijua” nilijisemea, niliwasindikiza kwa macho Caren na Ziada wakielekea ndani kwa ajili ya kutumia choo, nilipohakikisha kua walikua wameshaingia ndani, niliangaza huku na kule kama kuna Mtu yeyote aliyekua akimtazama yule Mzee, niligundua kila Mtu alikua bize na maongezi ya hapa na pale.
Nilishusha pumzi zangu kisha taratibu niligeuka na kuelekeza macho yangu getini, nilistaajabu kutomwoma tena yule Mzee
“Atakua ameenda wapi?” nilijiuliza, niliangaza huku na kule lakini niliambua patupu, haraka nikaelekea getini mahali ambapo palikua na umbali wa hatua zaidi ya ishirini kutoka eneo la Bustani ambako Palikua na tafrija.
Palikua kimya sana, niliangaza huku na kule, swali pekee lililozunguka kichwani kwangu nilijiuliza ni kwanini alikuja nyumbani kwetu, alialikwa na Nani, kwanini alikua akinitazama sana? Nani angenipa majibu ya maswali haya isipokua yule Mzee lakini yuko wapi, si getini wala karibu na eneo nililopo. Macho yangu yakaingiwa na shahuku ya kutazama nje.
Niligeuza shingo kuwaangalia wazazi wangu, walikua bize na wageni. Niliona ni bora nimtafute zaidi yule Mzee wa nyumba jirani. Hata nilipofungua geti hakuwepo, palikua kimya sana.
“Au atakua ameelekea nyumbani kwake?” nilijiuliza, bado kiu ya kutaka kumuuliza iliendelea kunishika, moyo wangu uligawanyika vipande viwili, kimoja kikiniambia niende nyumbani kwa yule Mzee haraka, kingine kiliniambia nitazungumza naye kesho. Kila nilichohitaji kukifanya nilijiona mzito sana, kwenda ndani au kuendelea na safari.
Kipande kimoja kiliishinda hii vita nzito ya dakika moja ya kusimama nje ya geti nikipigwa na Baridi. Nilipata ujasiri wa ajabu kuelekea nyumbani kwa yule Mzee, ilikua ni nyumba ya jirani, wastani wa hatua chache sana. Mbwa walikua wakibweka sana nyumba moja inayotazamana na nyumba yetu lakini sikuogopa.
Mwili ulinisisimka kwa kiasi fulani lakini sikujali sana, kila nilivyozidi kupiga hatua ndivyo mwili ulivyozidi kusisimka na kunipa hali ya hofu, mtaa ulikua kimya isipokua sauti ya Mbwa na Upepo fulani wa hapa na Pale, nilisimama na kuangalia nyuma. Hakuna Mtu, mbele hakuna Mtu, mi Mimi na fikra zangu, mapigo ya moyo yalianza kunienda mbio.
Niliweka pumzi sawa ili nizidi kusonga mbele, mara nilisikia sauti ya Caren.
“Celin, unaenda wapi?” sauti ilinishtua, sikutegemea kuisikia. Bado nilikua nimetazama mbele, nikakata shauri nikageuka. Caren alikua ameshanisogelea, mkononi alikua ameshikilia chupa ya Bia.
“What is wrong? ( Kuna tatizo?)” Aliuliza kwa udadisi wa hali ya juu, japo alikua amelewa kiasi lakini alionekana kuwa na wasiwasi, haraka niliachia tabasamu la kujibalaguza na kufanya dimpozi zangu zionekane.
“Aah‼ hapana, nilikua…yess‼ hakuna kitu, tunaweza kurudi ndani” niliamua kusema uwongo, sikutaka kumweleza yeyote yule juu ya wasiwasi wangu na hatua ninazozipiga. Bado mbwa alikua akibweka sana, tulipiga hatua za taratibu kurejea nyumbani huku nikiwa nina hisia kua kuna Mtu nyuma yetu alikua akitutazama.
Caren alisimama baada ya kuniona simjibu alichokua akinisemesha, nilianza kuhema kwa kasi, hofu ilikua imenitawala vya kutosha.
“Kuna nini Celin?” aliniuliza, nilimjibu Caren kwa sauti ya chini iliyojaa hofu na mtetemo wa Uwoga uliopitiliza.
“Kuna Mtu nyuma yetu” Nilitamani kulia kwa jinsi woga ulivyokua umenishika, Caren aligeuka nyuma kisha akarejesha macho kwangu. Akaangua kicheko na kuanza kuongea kama mlevi .
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya Pili
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx
17 Comments
Wa kwanza miee admin
Kuna mtu nyuma yetu…itakuwa wew admini
Nzury sana sehem ya pili jmn😅
Nzuri
Riwaya ni ya 🔥🔥
Very good story
Noma sana
Kaliii
Hatar
Uhuuuuuuuuu….❤️🔥❤️🔥❤️🔥❤️🔥❤️🔥
Add more
Mambo ni 🔥🔥🔥
Nzuri
Very good https://shorturl.at/2breu
🔥🔥🔥🔥✊
Nazipenda simulizi kama hizi
Very good https://shorturl.at/2breu
Ya motooo