Ilipoishia Nyumba Juu Ya Kaburi 04
“Unamkumbuka Zena?” nilimuuliza, alionekana kutafakari kidogo kisha akaniuliza “Yule rafiki yako?”
“Ndiyo!”
“Kimetokea nini?” aliniuliza kwa shahuku kubwa sana, sura ya Mama yangu haikua na hatia lakini nilijiuliza maswali mengi, nilijiuliza kama kweli hafahamu chochote vipi kuhusu jana Usiku walipotoka kwenye lile shimo yeye na Baba, wana uhusiano gani na Mwanamke anayelia kwenye ile stoo? . Endelea
SEHEMU YA NNE
“Amefariki Mama” nilisema kwa sauti ya kilio. Mama alishtuka sana kuliko kawaida, alishtuka kama vile alimfahamu Zena kwa muda mrefu sana, alishika kifua chake hadi nilishtuka
“Mama‼” nilimwita sababu namna alivyoipokea taarifa alikua kama amepandwa na presha. Alinitazama
“Pole Binti yangu, pokea rambirambi zangu” alisema kwa sauti ya upole sana kisha alisimama. Nilikua namtazama Mama yangu kama vile ilikua ndiyo mara ya kwanza namwona, alivyobadilika ghafla alizidi kunipa mawazo zaidi.
Simu yangu ilianza kuita tena, pochi yangu ilikua karibu na Mama yangu. Akanipatia Pochi, niliona ni bora niitoe simu niipokee, ilikua ni Namba ngeni. Kilichokua akilini mwangu niliwaza huwenda napewa ratiba za mazishi ya Zena, taratibu niliipokea na kuiweka sikioni bila kusema chochote, niliisikia sauti ya kiume ikiniuliza
“Wewe ni Celin?” moyo wangu ulifanya paaa kama nimewagiwa na maji, nilisimama “Eeh Ni Mimi!”
“Mimi ni Msamalia mwema, nimemsaidia rafiki yako Caren alikua amepata ajali mbaya sana jana Usiku. Yupo hapa Hospitalini, namba hii nimeikuta kwenye simu yake ndogo nikaona nikueleze kama unaweza kuja hapa Hospitali ya Jiji” Moyo wangu ulianza kunienda mbio, niliyakumbuka maneno ya Yule Bibi wa ajabu kua nitapoteza niwapendao kwa Mpigo.
Nguvu ziliniisha, nilijikuta nikiidondosha simu sakafuni kisha niliketi kitini kama mzigo. Macho yangu niliyaelekezea chini, chozi la ajabu lilinitoka. Nilijikuta nina hatia kubwa sana kwa kumshirikisha Caren kwenye hili jambo. Upepo ulianza taratibu huku ukipeperusha pazia, Mama yangu alinisogelea kwa utaratibu sana akaniuliza
“Kuna nini Celin?” nilimeza mate, nilikua kama Zezeta. Nilinyanyua macho yangu taratibu yakiwa yamejawa na uzito wa chozi lililoganda machoni pangu. Nilimtazama Mama yangu kama Mtu niliyepooza mwili mzima nikamwambia
“Caren‼” Mama alinitikisa kunirudisha kwenye ufahamu wangu lakini juhudi zake hazikufua dafu, uono ulinikimbia. Kila kitu nilikiona kipo mbali, hata pumzi zangu zilianza kunisaliti taratibu, niliona giza huku nikihisi ubaridi mwilini mwangu. Nilipoteza fahamu mikononi mwa Mama yangu.
****
Nilianza kusikia sauti inayofanana na kengele, sauti ilizagaa kichwa kizima. Ghafla nilishtuka, nilizinduka kutoka Usingizini. Mwili ulikua unauma, nilikua mchovu sana. Niliangaza huku na kule, niligundua nilikua kwenye chumba cha Hospitali, nilikua kitandani. Macho yangu yalikutana na macho ya Baba yangu pamoja na Mama yangu.
Mmoja aliketi upande wa kulia na mwingine aliketi upande wa kushoto, wote walionekana kunisubiria niamke. Nilipotaka kujitingisha Baba yangu alinizuia
“Taratibu Celin” alisema kwa sauti ya kujali sana. Hakuna kilichokua kimbebadilika kichwani kwangu. Nilijiuliza kama nilikua nawafahamu vyema wazazi wangu, nilitikisa kichwa kwa mbali kua nilikua sijawafahamu vizuri wazazi wangu. Hapo hapo niliikumbuka sababu ya Mimi kuwepo Hospitali, ni simu ile niliyopigiwa kuhusu Caren
Nilihema kwa uchovu, halafu nikamtazama Mama maana yeye ndiye aliyekua na Mimi wakati napoteza fahamu.
Mama yangu aliyasoma Mawazo yangu akawa wa kwanza kusema.
“Celin‼” aliniita Mama, niliiona sura yake ilivyojaa upole na unyongefu uliopitiliza, alituma ujumbe kwa sura yake nikajua fika kua Caren alikua amefariki kutokana na ile ajali, Mama yangu alinitazama kwa jicho la kunipa pole. Alikua akipepesa macho yake, aligeuza shingo na kumtazama Baba yangu.
Baba naye aligeuza shingo yake na kunitazama, alikua na sura ile ile aliyonayo Mama yangu. Sura zao zilikua zimejaa huzuni na huruma. Baba alinishika mkono wangu uliokua una sindano iliyotumika kunipatia maji mwilini.
“Celin, pole sana. Umepoteza marafiki wawili ndani ya siku mbili” alisema Baba kwa sauti ya Upole sana, sura yake ilijaa huruma sana. Hawakuonekana kama wana hatia lakini kwanini walikua kwenye lile shimo kule stoo, kuna uhusiano gani kati yao na yule Mwanamke anayelia. Swali hili lilihitaji majibu ya haraka, siyo rahisi wao wakanipatia Majibu.
Chozi lilianza kunidondoka, macho yangu yalianza kuwasha taratibu huku chozi likidondoka taratibu. Zena na Caren walikua marafiki wazuri kwangu lakini kila kitu kiliharibika baada ya Wazazi wangu kununua nyumba Mjini.
“Celin Binti yangu, najua unavyojisikia. Kupoteza uwapendao kunaumiza sana” alisema Mama yangu akinitazama kwa sura ile ile. Niliitikia kwa kutumia kichwa changu, sauti haikutoka kabisa. Nilijihisi ni mwenye hatia, Caren alikufa kwasababu yangu kama ningemzuia asiondoke Usiku ule basi asingepata ajali iliyopelekea kifo chake. Nililia sana lakini sikuwa na uwezo wa kurudisha wakati nyuma.
Mchana wa siku hiyo niliruhusiwa kutoka Hospitalini, nilirudishwa nyumbani na Wazazi wangu. Mwili ulikua na uchovu sana, sikuweza kwenda Kumzika Zena maana alizikwa nikiwa Hospitali, hata Sikuwahi kwenda kuuaga mwili wa Caren ambao ulisafirishwa mara moja kuelekea Mji wa Wazazi wake ambako ndiko wanakozikia ndugu zao.
Nilibakia nikiwa mpweke kuliko wakati wowote kwenye Maisha yangu. Mama yangu alinitazama kwa ukaribu sana kwa siku mbili hadi alipothibitisha kua akili yangu ilianza kutulia.
Sikupata majibu ya maswali yangu hata pale niliporudi tena kule stoo sikuliona lile shimo, sauti ya Mwanamke anayeimba nayo ilitoweka kabisa
**
Zilipita siku kadhaa, nilianza tena kwenda chuo. Maisha yaliendelea bila Zena na Caren, Wanachuo wenzangu walinipa pole kwa kuondokewa na marafiki wawili niliowapenda.
Usiku mmoja nikiwa nimelala chumbani kwangu, nilianza kupata njozi ya ajabu sana. Niliota nikiwa ninalia halafu pembeni yangu kuna Mtu aliyejifinika shuka gubi gubi akiwa hatikisiki. Nililia sana, chozi lilinitoka huku nikiwa nimejawa na uchungu sana, njozi hii ilikua ikitokea
ndani ya chumba kimoja chenye kitanda cha Hospitali, Mtu aliye juu ya Kitanda alikua amefunikwa shuka jeupe.
Nilikua ninalia huku nikisema
“Usiniache nitabaki na Nani Mimi, usiende nakuomba rudi” Sijui nilikua namlilia Nani, ghafla nilishtuka kutoka Usingizini,niliketi nikiwa nina pumua haraka haraka. Chumba changu kilikua giza kidogo, nilisimama baadaye na kuwasha taa. Japo nilipata ndoto ya kutisha lakini Usingizi ulikua mwingi machoni pangu
Nilijivuta ili nielekee chini kupata maji ya kunywa, nilijifunga vizuri nguo yangu ya kulalia, wakati nauelekea Mlango nilianza kusikia sauti ya Mwanamke mmoja, ilikua ni sauti ile ile ya Mwanamke anayeimba lakini safari hii alikua akilia, nilishtuka sana. Nilipigwa na Butwaa huku nikisikia vyema kua ilikua ikitokea nje ya Mlango wa chumba changu.
Hata mate hayakuweza kupita kooni kwa jinsi ambavyo nilikua nimejawa na hofu, nilitamani kugumia kuwaita Wazazi wangu lakini sikuweza, butwaa iliyokua imeniingia akilini ilinifanya nitulie kimya nikisikiliza ile sauti. Wakati naendelea kuisikiliza ile sauti nilianza kuhisi ilikua ni sauti ya Mtu ninaye mfahamu
“Mamaaa‼” nilipata jibu, ilikua ni sauti ya Mama yangu Mzazi. Alikua akilia kisha alianza kuniita jina langu. Hofu ilizidi kuniingia, nilisimama nikiwa ninaangalia sana mlangoni. Nilitamani kumwita Mama na kumuuliza analia nini lakini nilipokumbuka nilichokiona Usiku ule nikiwa na Caren niliishiwa nguvu kabisa.
Aliendelea kulia huku akiniita kwa jina langu hali iliyoizidi kunichanganya, mwendo wa dakika tano tu kisha sauti ya Kilio iliondoka Mlangoni kwangu, nikawa naisikia ikishuka chini kupitia ngazi. Chozi lilinilenga sababu sikujua anayelia kama alikua ni Mama yamgu kweli na kama ni Mama yangu basi ndiye anayeleta Mauzauza.
Baada ya sekunde kadhaa ile sauti ilitoweka, palikua kimya sana. Sikupata Hata lepe la Usingizi, nilikesha nikiwa macho. Asubuhi mapema niliamka na kujiandaa kisha niliondoka nyumbani bila hata kuwaaga wazazi wangu, nilimpigia simu yule Dalali ili nimuulize maswali kadhaa, nilikua na uhakika hata yeye alikua anajua ni nyumba ya aina gani aliwauzia Wazazi wangu.
Wakati natoka niliitazama sana nyumba ya yule Mzee jirani, ilikua tulivu sana. Majani makavu yalikua yameanguka sana uwani kwake kuashiria kua palikua hapakaliwi na Mtu yeyote yule
Nilimpigia simu kwa namba ngeni, nilikua na uhakika kama angelijuwa ni Mimi asingelinipa ushirikiano wowote ule. Nilimwambia kua nahitaji chumba cha kupanga, akanitajia mahali alipo huku akinisistiza kuwa niende hapo akanioneshe chumba kizuri. Kama kawaida yangu nilikua napendelea sana treni sababu ya kukwepa usumbufu.
Baada ya kufika eneo ambalo tulikubaliana tukutane, yeye sikumkuta hapo. Niliangaza huku na kule lakini sikufanikiwa kumwona, niliketi mahali nikimsubiria huku nikijaribu kumpigia simu lakini simu yake ilikua haipokelewi kwa zaidi ya dakika tano, mwanzo niliona ni jambo la kawaida lakini baadaye nilipata hisia ya tofauti.
Nusu saa nzima simu yake ilikua haipokelewi kisha baadaye ilizimwa kabisa. Mahali alipokua amenielekeza palikua ni Kijiwe cha kahawa, hapo ndipo anapopatikana kwani hata mara ya kwanza nilikutana naye hapo. Nilikata shauri la kuendelea kumsubiria hapo, nilinyanyuka na kuuvaa mkoba wangu ili niondoke
Mara akaja Mwanaume mmoja aliyekua akiendesha Pikipiki kwa kasi sana, japo alikua haji upande wangu lakini mwendo wake Ulinifanya niwe macho kumtazama. Aliegeshe Pikipiki kando kidogo ya kundi la Wanaume walioizunguka meza ya kahawa kisha akaketi huku akisikitika kama Mtu aliyepoteza Umakini wake.
Nilinogewa na kuwatazama. Nilisimama nikiwa sikwepeshi macho yangu huku masikio yangu yakiwa kama antena, walianza kumuuliza kwanini alikua katika ile hali ya kuchanganikiwa, akawa anajisonya-sonya tu huku akishikilia kichwa chake, walianza kumzingatia hata kwa wale walioanza kuhisi ulikua ni utani walianza kuweka Umakini huku wakizidi kumuuliza
“Sheby jamani‼” alianza kusema huku akihema sana.
“Sheby amefanya nini?” aliuliza mmoja wao akiwa anamtikisa bega, walionekana kumjua huyo Sheby na pengine alikua ni Mtu wao wa karibu.
“Sheby eeeee haaaaa‼” alitoa sauti kubwa iliyoambatana na kilio
“Sheby amefanya nini?” aliuliza mwingine, shahuku ikazidi kuwa kubwa, siyo kwao tu hata kwangu. Taratibu nilianza kupiga hatua ndogo za kuhebu ili nisikie neno.
“Amekufaa‼ ajali jamani aaaah Maisha hayaaa‼!” yule Mwanaume alizidi kuendelea kulia, Watu walisikitika sana kusikia taarifa za kifo cha huyo Mtu, papo hapo akili yangu ikakaa sawa‼ Yes, Dalali niliyewasiliana naye anaitwa Sheby. Nilihisi mwili kama unatengana na roho yangu Jamani, nilikua na tumaini la kupata majibu ya maswali yangu kwa huyo Sheby halafu ghafla nasikia taarifa ya kifo chake.
Niliishiwa nguvu, nikasogea na kuketi juu ya gogo moja. Ndiyo maana simu zangu zilikua hazipokelewi, nilipata mfadhahiko mkubwa sana. Chozi lilikua likinimwagika, nilijuwa kua kuna
jambo lisilo la kawaida linaloondoa uhai wa Watu wasio na hatia, moyo wangu ulivunjika vipande vipande hata ile nguvu niliyokuja nayo ilipungua kabisa.
Nilitazama juu huku chozi likizidi kunibubujika kutoka machoni kuteremka hadi mashavuni kisha kwenye gauni langu, nilihisi Dunia ikizunguka. Nilikosa majibu ya maswali yangu yote, Uchungu ulipanda kutoka kifuani niliuhusi ukija hadi puani na kunipa maumivu makali sana. Hali ya mafua ya ghafla ilianza pale pale nikiwa bado kichwa changu kimeelekea juu.
Imani ya moyo wangu iliniambia kua Mungu alikua angani akinitazama kila hatua lakini hakutaka kunisaidia, nilisema ndani ya Moyo wangu.
“Eeh Mungu, nitapoteza wangapi? Hii ni ndoto, niamshe basi nikutane na wapendwa wangu” niliumia sana ndani ya moyo wangu, Mungu aliniachia mizigo yote niibebe mwenyewe katika wakati mgumu ambao kila niliyemshilisha alikufa kifo cha ghafla. Nilipoteza Watu watatu, mmoja ni dalali niliyeamini alikua akiyajua mazingira ya nyumba yetu na wengine ni marafiki zangu wawili niliowapenda kama nilivyozipenda mboni za macho yangu.
Ghafla nilisikia sauti kando yangu, nilishtuka. Ilikua ni sauti ya kiume iliyoanza kwa utaratibu sana kisha kuniachia tabasamu la mwongeaji.
“Pole, haijalishi unapitia nini kwenye Maisha yako. Mungu atashinda na wewe” niligeuka haraka kumtazama aliyeongea, alikua upande wangu wa kulia, ni Mwanaume mwenye ndevu nyingi, mtanashati aliyenizidi Umri lakini alikua rika langu.
Nilisogea pembeni haraka kwa hofu maana sikutaka kumwamini Mtu yeyote yule.
“Usiogope Celin‼” Mungu wangu, alinifahamu kwa jina. Hii siyo tu ilinishtua pia iliniacha na Butwaa la ajabu sana, nikamkumbuka yule Bibi wa Ajabu ambaye alinisemesha kwenye treni na kuanzia hapo kila kitu kiliharibika.
“Tafadhali kaa mbali na Mimi, hunijui sikujui. Jina langu siyo Celin” nilisimama kisha nilipaza sauti yangu, kila mmoja aliye jirani na sisi alitutazama kwa Mshangao na maswali mengi. Yule Mwanaume wala hakujali, aliendelea kutabasamu na kunidhihirishia kua alikua Mtu wa ajabu kama yule Bibi.
Niliondoka hapo haraka huku akiniita kwa jina langu akidai napaswa kumsikiliza, sikutaka hata kugeuka nyuma, niliyaziba masikio yangu ili hata kumbukumbu ya Sauti yake isibakie masikioni mwangu.
Nilipofika barabarani nilisimamisha Taxi ya njano kisha haraka nikaingia na kuketi siti ya nyuma kisha nikamuamuru dereva aondoe gari anipeleke chuoni, hapo chozi lilikua likinibubujika. Bado sauti yake ilikua inasikika masikioni mwangu. Maneno ya yule Mwanaume yalikua yakijirudia.
“Endesha haraka” nilisema kwa sauti ya juu ili dereva aongeze mwendo, nilikua nimegubikwa na woga wa ajabu, hofu na Mashaka vilikua vimenitawala kwa kiasi kikubwa sana. Nililia kama
Mtoto mdogo, sikujua nilikosea kuichagua ile nyumba au kuna mahali familia yangu ilifanya kosa na sasa tunaadhibiwa.
Dereva aliongeza mwendo kama ambavyo nilikua nimemwambia. Nilikua nimejiinamia nikiwa nimeziba masikio yangu, taratibu ile sauti ilianza kupotea masikioni mwangu. Zilipita dakika kadhaa ambazo zilitosha kwa dereva kukaribia chuoni. Nilijihisi nafuu sana, kisha nilitoa kitambaa na kujifuta chozi kisha nilifuta pua zangu.
Niliponyanyua Sura yangu nitazame nje nijuwe kama tulikua tunakaribia chuoni au laa, nilipigwa na Butwaa nyingine. Nje ya gari palikua na Msitu mkubwa sana, halafu gari lilikua likitembea kwa mwendo wa kawaida.
Nilipaza sauti yangu “ Wewe dereva umenileta wapi huku?” nilisema huku nikijaribu kufungua mlango lakini ulikua umefungwa. Hofu niliyoiacha ilianza kunivaa upya halafu nikaisikia sauti ile ile ya yule Mwanaume niliyemkimbia akisema
“Haijalishi unapitia nini, kumbuka maneno yangu. Utashinda” Masikini, yule dereva alikua ni yule Mwanaume niliyemkimbia, aliwezaje kuingia ndani ya gari sijui, nitamkimbia vipi sijui na kwanini anajua kila kitu kuhusu Mimi pia sijui.
Nilikua ninatetemeka sana. Kisha lile gari likachepuka kutoka barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi iliyo kimya sana, hapakua na yeyote.
“Wewe ni Nani?” nilimuuliza nikiwa ninalia, nilijua haiwezekani tena kumkimbia. Kwa namna alivyo siyo rahisi pia kupambana naye. Alisimamisha gari kisha aligeuka na kunitazama, sura yake ilionesha alikua na jambo kubwa analohitaji kuniambia.
Alinionesha sura ambayo haikua na hatia, wala hakuonesha kama alikua na nia ya kunifanyia jambo baya, kisha kwa sauti ya taratibu aliniambia
“Usiniogope Celin, nahitaji Msaada wako. Nitakusaidia pi, tusaidiane” kauli hii ilianza kunipa tumaini la kuishi tena, kama alihitaji msaada wangu asingeliweza kunidhuru lakini haraka haraka akiwa ananiangalia nilijiuliza alihitaji Msaada gani kutoka kwangu wakati yeye anaonekana kua ni Mtu wa ajabu ajabu kama yule Bibi.
Nilibabaika kumjibu, sauti ilitoka kwa wasiwasi tena isiyo na nguvu. “Nikusaidie nini? Tafadhali usidhuru Maisha yangu” nilisema huku nikiwa ninalia, niliweka mikono yangu kifuani kwangu kwa isharaka ya kumwomba ahurumie Maisha yangu, alikuwa akinitazama nusu bega huku mwili wake wote ukitazama mbele.
“Ningekua na nia ya kuyadhuru Maisha yako ningefanya hivyo muda mrefu, nina ombi moja tu kwako Celin” Maneno ya yule yalianza kunipa tumaini zaidi na zaidi kua pengine nitapata nafasi nyingine ya kuishi, alionesha wazi kua alikua akinifwatilia kwa muda mrefu sana.
“Nitakusaidia nini Mimi Kaka yangu?” nilimuuliza, angalau swali hili lilitoka huku nikiwa nimetuliza kilio changu.
Alikunja midomo yake, ishara hii iliniambia ndani yangu kua alihitaji kuzungumza jambo zito sana, alitafakari huku akinitazama akiendelea kukunja midomo yake. Halafu akaniambia “Nataka umtoe Dada yangu ndani ya nyumba yenu”
“Dada yako?”
“Ndiyo!”
“Kivipi, ni yupi mbona sisi tunaishi watatu, Mimi na Wazazi wangu?” nilimuuliza huku moyo wangu ukiamini kua nilikua karibu kugundua siri fulani ya nyumba yetu. Alishusha pumzi zake kisha akaniambia
“Teremka kwenye gari, nitakueleza zaidi. Najua una maswali mengi sana” alisema kisha alifungua mlango wa gari kisha aliteremka na kusimama mbele ya gari akiegemea ‘Boneti’
Nilikua ninamtazama kwa makini nikiwa bado nina jishauri kama nitaweza kumwamini Mtu nisiyemjua, lakini niliuvaa ujasiri wa ghafla kisha niliufungua mlango kirahisi sana, mlango uliokua Mgumu hapo awali, safari hii ulifunguka nilipoutekenya.
Sekunde kadhaa nilikua nikiivuta hewa ya jua kali lililokua likiwaka nje, niliyatazama mazingira tuliyopo. Niliona miti mingi iliyofungana, tulikua msituni japo kwa mbali nilisikia sauti ya magari yakitembea kwa kasi. Upepo wa taratibu ulikua ukiendelea na kufanya eneo hilo kua na hali mbili tofauti. Jua kali lakini pia upepo uliopoza joto kali
Taratibu nilitembea kuelekea mbele ya gari kumsikiliza yule Mwanaume, alikua mnene kiasi na pia alikua na ndevu nyingi mfupi wa wastani, alikua ananukia manukato makali sana. Nilitembea taratibu huku nikijikwaa jiwe dogo lililonipa mwendo zaidi hadi nilisogea kabisa karibu yake, akanipa pole huku akigeuka na kunitazama nikitembea taratibu hadi nilipofika mbele yake.
“Usiwe na wasiwasi Celin, usiogope sababu nusura ya Maisha yenu yapo mikononi mwako” niliyafinya macho yangu kwa mshangao mkubwa sana, moyo ulilipuka ghafla na kuanza kwenda mbio
“Unamaanisha nini?” nilimuuliza nikiwa na mhemko wa alichoniambia, tayari nilikua nimepoteza marafiki zangu wawili.
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya SITA
COMMENTS ZIWE NYINGI SASA
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx
1 Comment
Nzuri dah