Ilipoishia Sehemu Ya 3 Nyumba Juu Ya Kaburi
Hata nilipojaribu kufurukuta sikuweza kisha nikaisikia sauti ya Caren
“Shii‼ ni Mimi” aliongea kwa sauti ya kunong’oneza. Aliniachia, hapo hapo kabla sijamuuliza alifikaje, sote tulimwona Yule Mzee akiwa ameshikilia tochi, alikua akichungulia pale mlangoni nilipotaka kuingilia, kwa namna nilivyomwona ni kama alihisi uwepo wa Mtu. Alimulika tochi huku na kule lakini hakufanikiwa kutuona kisha aliufunga mlango wa Nyumba yake.
Hapo tuliachia pumzi ndefu maana tulikua tumezibana kuhofia asije akatushtukia. Endelea
SEHEMU YA NNE
“Unafanya nini hapa?” nilimuuliza Caren, sikutegemea angefika pale maana nilimpigia simu lakini hakushika simu yangu. Nilimuuliza kwa sauti ya chini sana, akanijibu
“Tutoke hapa Celin, turudi nyumbani kwenu tafadhali” ilionekana mpango wangu umeshindwa kufanya kazi usiku huu, basi taratibu tuliondoka. Tulilipanda lile geti tukatua upande wa pili kisha tulirudi nyumbani.
Tuliingia hadi chumbani kwangu, Nilikua na maswali mengi kwake. Alinitazama kwa sekunde kadhaa kisha akaniambia
“Celin nashindwa kukuelewa, umenitumia ujumbe na kunieleza mahali ulipo ndiyo maana nilikuja, unaniuliza nimefikaje?” Nilitikisa kichwa changu, maneno ya Caren yalikua kama yamejaa mzaha hivi
“Mimi?” nilimuuliza huku nikiwa najipiga kifuani.
“Caren, nilipiga simu yako hukushika. Sikutuma ujumbe wowote ule” Caren alitikisa kichwa chake akionesha wazi kua alikua akimaanisha alichoniambia, kisha alitoa simu yake na kunionesha ujumbe ambao alidai nilimtumia, ni kweli namba yangu ilionesha kumtumia ujumbe Caren. Macho yalinitoka, niliyapepesa huku nikihakiki. Funda zito la mate lilikua likipita kooni kwangu
“Caren, hali inaweza kua mbaya zaidi. Haya ni maajabu ya Dunia, sijakutumia ujumbe kama huu. Nina hisia kuwa kuna mchezo wa kichawi unafanyika” nilisema.
“Wakati nakupigia simu nilisikia kitu cha ajabu sana chumba cha chini, hii nyumba inaweza kua na mizimu Caren. Unaweza ukaniamnini?”
“Celin, kama unahisi hivyo ni bora ukawaambia Wazazi wako kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. Sisi hatuwezi kupambana na hizo nguvu” alisema Caren, sura yake ilijaa hofu na woga sana, nilimuelewa. Nilimshika mkono nikamwambia huku nikimtazama usoni
“Baba yangu ana presha, sitaki kumtia matatizoni zaidi. Pesa yote ya kustaafu ameinunua hii nyumba. Nikimwambia ninaweza nikampoteza Caren, tafadhali tutafute ufumbuzi” nilimsistiza Caren, yeye alikua ndiye Mtu pekee niliyemueleza kuhusu nyumba hii mpya na mauza uza yake. Alitikisa kichwa akiitikia japo alikua na woga
“Tunaweza kwenda chini? Nilisikia sauti ya Mwanamke akiimba kutokea stoo, pengine tunaweza kupata majibu huko” Bado nilikua nimejawa na shahuku sana. Caren aliitikia kwa
kutumia kichwa huku jasho likimtiririka, basi tuliongozana kushuka ngazi taratibu hadi tulipofika chini, palikua giza sababu taa zote zilizimwa.
Pumzi za Caren zilikua juu sana, alikua akihema kama Mtu aliyetoka kukimbia, hofu ilimjaa sana. Nikamwambia
“Usiogope Caren, hakuna tulichokosea hatustahili kuadhibiwa. Twende” nilisema, Binafsi nilikua na Ujasiri sana, sikutaka tuwashe taa sababu sikutaka Mama anikute tena pale pale aliponikuta na kuniuliza maswali. Miili yetu ilianza kusisimka kadili tulivyoisogelea stoo.
Hatua kadhaa mbele tulianza kusikia tena sauti ya Yule Mwanamke akiimba, ilikua ni sauti nyororo sana ikitokea stoo. Hatukuelewa alikua akiimba nyimbo gani wala lugha aliyoitumia kuimba hatukuijua. Hofu ilianza kuniingia lakini ilikua ni lazima nipate majibu ili kuwaokoa niwapendao.
Tulisimama tukiendelea kumsikia akiimba, ilionekana alikua ametulia sana, sauti yake ilikua ya taratibu iliyojaa upweke fulani ndani yake. Miili ilizidi kusisimka, hadi tunafika mlango wa stoo tulikua na miili mizito ambayo tuliisukuma kwenda mbele, msisimko ulikua wa ajabu sana ambao sikuwahi kuuhisi kabla yake.
Palikua na mwanga hafifu sana kutokea nje kupitia dirishani pale kwenye korido, taa ya nje ndiyo iliyokua ikiendelea kutupatia uelekeo. Niliuvuta mkono wangu huku nikisema liwalo na liwe, japo mkono ulikua mzito lakini nilifanikiwa kutekenya kitasa, mlango ukafunguka.
Pakawa kimya sana, hatukuisikia tena ile sauti ya Mwanamke akiimba, wala ile hali ya kusisimka mwili ilikua imetoweka, ni kama tulikua tumevuka kizingiti kizito mbele yetu, nilikua wa kwanza kuingia stoo kisha nilipapasia na kuwasha taa, mwanga wa taa ukakita kila kona ya chumba cha stoo. Humo tulihifadhi baadhi ya vitu ambavyo hatuvitumii tena, vilikua vimetokea Kijijini na vingine tulivikuta baada ya kuhamia.
Chumba cha stoo kilikua kikubwa sana, kilikua na hewa, eneo kubwa la kuhifadhi vitu zaidi na zaidi. Caren naye aliingia akiwa anaogopa, nilianza kutafuta mahali ambapo ile sauti ilitokea, hapakua na yeyote ndani ya kile chumba.
“Si uliisikia sauti Caren?” nilimuuliza, alimeza mate kwanza kisha alinijibu akiwa bado anaendelea kuogopa
“Ndio ilitokea humu, Celin….” Caren alinionesha kitu nyuma yangu, palikua na kitu kilichonifanya nigeuke kwa haraka sana. Palikua Na shimo ambalo wakati tunaingia hatukuliona, istoshe hata wakati tunaweka vitu stoo hatukuliona.
Shimo hilo lilikua kama njia ya kushuka chini, tulisogea na kuchungulia, palikua na ngazi za kuelekea chini. Nilimtazama Caren, macho yetu yaligongana, tulikua na maswali mengi sana yasiyo na majibu.
Mara tulisikia vishindo vya miguu ikipanda kutoka chini kuja juu, shimo lilikua na giza. Mimi na Caren tukajificha nyuma ya pipa huku macho yetu yakikodolea shimo lile Kuona ni Nani aliyekua akitokea humo, tulijawa na hofu kiasi kwamba tulikua tukitetemeka. Macho yetu yalikua eneo hilo tena kwa shahuku kubwa sana.
Kila hatua ilizidi kutupatia hamu ya kuona ni Nani aliyekua akitoka ndani ya shimo hilo, nilichokua nafikiria ni kumwona Mwanamke anayelia ambaye sauti yake niliisikia zaidi ya mara moja. Moyo wangu ulizidi kupiga kwa hofu na wasiwasi usio na ukomo, hali hiyo ilikua kwa Caren pia, yeye alikua akitetemeka kabisa.
Ghafla palikua kimya, hazikusikika tena zile hatua. Mimi na Caren tulitazamana kwa mshangao mkubwa sana, bado macho yetu yalikua yakitazama eneo lile lenye shimo. Mara tuliona Kichwa, kisha mwili, Mungu wangu alikua ni Baba yangu tena akiwa uchi wa Mnyama kama alivyozaliwa, alifuatiwa na Mama yangu ambaye naye alikua kama Baba yangu.
Mshangao mkubwa uliniingia, cha ajabu ambacho kilizidi kunishangaza ni namna walivyo, walikua Uchi lakini walikua wamefumba macho yao kama watu wanaotembea wakiwa Usingizini. Hawakutazama popote kisha waliongoza kuondoka ndani ya chumba, halafu pale shimoni palijifunga.
Nilimziba mdomo Caren maana alikaribia kupiga kelele za hofu, nilimtaka akae kimya kisha nilimwambia tuwafuatilie wazazi wangu. Taratibu tulianza kiwafuata kwa nyuma, hatua kwa hatua hadi walipoingia chumbani na kufunga mlango
Walituacha na maswali mengi yaliyokosa majibu, tulirudi chumbani kwangu. Sikutaka kuamini hasa nilichokiona, Caren alinifuata niliposimama kisha aliniuliza
“Ina maana wazazi wako wanalijua hili jambo na wameamua kukaa kimya, au ni washirika?” aliniuliza swali lililozidi kunipa maumivu sana, chozi lilinidondoka nikifikiria Nilichokiona, nilitamani iwe ndoto niamke lakini lilikua tukio la kweli lililoniacha na maswali mengi sana kichwani, nilifikiria namna ambavyo Mama alinizuia nilipokua nafuatilia sauti ya Mwanamke anayeimba.
Uchungu ulikishika kifua changu, jasho lilinitoka huku chozi likinibubujika, sikujua nimpe jibu gani Caren, tulimpoteza Ziada katika mazingira ya kutatanisha. Nani ana majibu ya maswali yetu? Ni yule Mzee wa nyumba jirani, yule Bibi wa ajabu au Wazazi wangu?
“Celin, siwezi kubakia hapa naondoka. Nina hisia mbaya sana juu ya wazazi wako, tulicho kishuhudia hakikua kitu cha kawaida” alisema Caren. Nilimuelewa, hata kama ningekua kwenye nafasi yake ningefanya hivyo hivyo lakini Mimi siwezi kuikimbia nyumba yetu. Niliishia kumtazama Caren akiwa anatokwa na machozi alichukua mkoba wake na kuishia zake, nilizisikia hatua zake akishusha ngazi.
Sikuweza kumzuia, moyoni mwake aliamini wazazi wangu walikua wachawi na hata mzizi wa kifo cha Zena ulitokana na Nyumba yetu, kuwaona wazazi wangu katika hali ile aliamini kua
kuna jambo walikua wanalijua na waliamua kulificha. Nilibakia nikiwa nimeketi kitandani nikiwa ninalia
Nilikua na usiku usiosahaulika Maishani mwangu, kila nilivyowafikiria wazazi wangu chozi lilikua likinibubujika bila kupumzika. Nilifuta chozi kila dakika hadi kulipopambazuka, asubuhi ilinikuta nikiwa nimeketi kwenye kochi chumbani kwangu.
Simu yangu ilikua ikiita sana, tena iliita mfululizo lakini sikutaka kujua nani anapiga wala sikua na mpango wa kuipokea, niliiacha iite hadi ilipokata yenyewe. Hisia za Usiku ziliendelea kunitesa, mara nilisikia mlango ukigongwa
Sikuitikia wito wa hodi hiyo, niliishia kuutazama mlango. Kisha ulisukumwa na kufunguka, nilikumbuka mlango sikuufunga. Mama yangu alikua amesimama mlangoni akinitazama, chozi lilianza kunilenga lakini sikutaka kuliruhusu lidondoke, Mama alisogea karibu nami, akaketi kitandani huku akionekana kunishangaa
“Hujaniona?” aliniuliza, nilimtazama Mama kisha nilimjibu
“Samahani Mama, kichwa changu hakipo sawa. Shikamoo” nilisema, sikutaka kumuuliza chochote kuhusu Usiku uliopita.
“Marahaba Celin, kimetokea nini?” Swali hili nusura chozi linidondoke, nilihisi Mama yangu alikua akiuliza jambo analolifahamu. Niliumia ndani yangu sababu ni Mama yangu Mzazi, nilipepesa kope za macho yangu kama Mtu anayekaribia kulia
“Sio sawa Mama, nahisi nipo kwemye Dunia iliyojaa siri, isiyo na huruma kabisa. Sijui kwanini siambiwi ukweli Mimi” Kusema ule ukweli nilijikuta nikidondosha chozi langu, Zena alijaa mawazoni, Mama alinishika bega akaniuliza
“Kimetokea nini Celin, niambie Mimi ni Mama yako?” aliongea kwa kusisitiza huku sura yake ikionesha kutokua na hatia, alionesha kutofahamu chochote kile. Niliziweka nywele zangu vizuri maana zilivurugika kutokana na purukushani za Usiku, chozi liliendelea kunibubujika nikamtazama Mama huku nikiwa ninafuta chozi langu
“Unamkumbuka Zena?” nilimuuliza, alionekana kutafakari kidogo kisha akaniuliza “Yule rafiki yako?”
“Ndiyo!”
“Kimetokea nini?” aliniuliza kwa shahuku kubwa sana, sura ya Mama yangu haikua na hatia lakini nilijiuliza maswali mengi, nilijiuliza kama kweli hafahamu chochote vipi kuhusu jana Usiku walipotoka kwenye lile shimo yeye na Baba, wana uhusiano gani na Mwanamke anayelia kwenye ile stoo?
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya TANO
COMMENTS ZIWE NYINGI SASA
JIUNGE NA KIJIWENI WHATSAPP CHANNEL Kwa Kugusa Hapa
Soma Riwaya Nyingine Za Kijiweni Kwa KUGUSA HAPA
Wewe kama MFANYABIASHARA.. Kuna wakati unatamani kuwafikia watu wengi zaidi na hujui wapi pa kuanzia , USIJALI kwani hapa ndipo ambapo MTAA UNAONGEA na tuko tayari kukusaidia kuwafikia watu wengi kwa BEI YA OFA
Njoo Utangaze Nasi Sasa Kwa Kutuambia Una TANGAZO Gani na unataka kutangaza kwa muda gani kwa kutuma ujumbe hapa WwhatsApp Kupitia Namba +255760871896
Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx Nyumba Juu Ya Kaburi xx
10 Comments
😭😭😭😭🤣🤣😭😭😭😭😭😭😭😭😭😭😭
🙆🙆
Oh jaman ☹️☹️☹️☹️🥺🥺🥺🥺
Uwe unatoa vipande viwili per day admin🤣🤣🤣🤣🤣
Dah leo kafupi
Duh
Wow nzur sana
ongeza frequency admin iwe kila siku😁😁
Kaz ipo
Story nzuri sana